MFUMUKO WA BEI WA TAIFA WAPUNGUA HADI ASILIMIA 6.1
Mkurugenzi wa
Sensa ya Watu na Takwimu za Jamii wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Ephraim
Kwesigabo akiongea na wanahabari kuhusu Mfumuko wa Bei wa Taifa wa mwezi
Mei 2017 jijini Dar es Salaam leo.
MFUMUKO wa Bei wa Taifa kwa mwezi Mei, 2017 umepungua hadi
asilimia 6.1 kutoka asilimia 6.4 ilivyokuwa mwezi Aprili, 2017.
Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam leo
Mkurugenzi wa Sensa ya Watu na Takwimu za Jamii, Ephraim
Kwesigabo amesema kupungua kwa mfumuko wa bei kunatokana na kupungua kwa kasi
ya upandaji wa bei za bidhaa na huduma ikilinganishwa na kasi iliyokuwepo kwa
mwezi Aprili, 2017.
“Mfumuko
wa Bei wa Taifa umepungua kutoka asilimia 6.4 kwa mwezi Aprili, 2017 hadi
kufikia asilimia 6.1 kwa mwezi Mei , 2017 kutokana na kupungua kwa kasi ya
upandaji wa bei za bidhaa na huduma kwa mwezi Mei, 2017,” amesema Kwesigabo.
Kwesigabo
amesema Mfumuko wa Bei wa mwezi Mei, 2017 unaopimwa kwa kipimo cha mwezi
umeongezeka kwa asilimia 0.2 ikilinganishwa na ongezeko la asilimia 0.5
ilivyokuwa mwezi Aprili, 2017.
Amesema
Fahirisi za Bei zimeongezeka hadi 109.26 kwa mwezi Mei, 2017 kutoka 109.04
mwezi Aprili, 2017 kutokana na kuongezeka kwa bei za baadhi ya bidhaa za
vyakula na zisizo za vyakula.
Kwesigabo
ametaja bidhaa za vyakula zilizochangia kuongezeka kwa fahirisi kuwa ni pamoja
na mahindi yaliyoongezeka kwa asilimia 4.2, maharage mabichi kwa asilimia 2.9,
maharage ya soya kwa asilimia 2.2, unga wa mtama kwa asilimia 1.5, viazi
mviringo kwa asilimia 2.0, mihogo mikavu kwa asilimia 2.3, na magimbi kwa
asilimia 2.5.
Aidha
bidhaa zisizo za vyakula zilizochangia kuongezeka kwa fahirisi za bei ni pamoja
na mkaa ulioongezeka kwa asilimia 2.5.
Ameongeza
kuwa Mfumuko wa Bei kwa bidhaa za vyakula nyumbani na migahawani kwa mwezi Mei,
2017 umepungua hadi asilimia 11.8 kutoka asilimia 12.0 mwezi Aprili, 2017.
Aidha, badiliko la Fahirisi za Bei kwa bidhaa zisizo za vyakula umepungua hadi
asilimia 3.0 mwezi Mei, 2017 kutoka asilimia 3.4 mwezi Aprili, 2017.
No comments