JENGO LA UPASUAJI KITUO CHA AFYA MIONO LASUASUA
JENGO la Upasuaji katika Kituo cha afya cha Miono, Halmashauri ya Chalinze ,Mkoa wa Pwani bado hakijakamilika, kutokana na changamoto hasa ya mkanganyiko wa matumizi ya fedha zinazoelekezwa kwenye ujenzi huo.
Hayo yamebainika katika ziara ya Kamati ya siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani, ilipotembelea miradi inayotekelezwa na Halmashauri hiyo, ikiongozwa na Mwenyekiti wa chama hicho Alhaj Abdul Sharifu.
Akitoa taarifa ya ujenzi wa Jengo hilo, Shaban Mpwimbwi ambae ndio Mwenyekiti wa Kamati ya Usimamizi wa ujenzi wa Kituo hicho, alisema kuwa awali zimepelekwa sh .mil.105, baadae Mil. 20 na kuwa jumla ya sh.Mil. 125, kumekuwepo na kauli tofauti kuhusiana na matumizi ya fedha.
Taarifa ya Mganga Mkuu wa Kituo cha afya Miono Rehema Derua ilielezea masuala mbalimbali yanayohusiana na ujenzi wa jengo hilo la upasuaji katika Kituo hicho, na kwamba mpaka sasa ukamilishwaji wake unasuasua.
Baada ya kupokea taarifa hiyo, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Bagamoyo Alhaj Abdul Sharifu alisikitishwa kusuasua kwa jengo la upasuaji, wakati wananchi wakiangaika katika kupata huduma ya matibabu yanayohusiana na upasuaji.
“Kamati yetu italifanyia kazi hili kuona kitu gani kinakwamisha kukamilika kwake, katika kamati yetu baada ya kumaliza ziara tutakuwa na kikao kitachohusisha Wakurugenzi wa Halmashauri zote mbili kwa maana ya Chalinze na Bagamoyo ,” alisema Sharifu.
Mjumbe wa Kamati hiyo Yahya Msonde, alishauri uchunguzi kuhusiana na matumizi ya fedha hizo ufanyike ikiwashirikisha watu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU ili kujiridhisha utekelezaji wake.
No comments