Header Ads

click here

KAMPUNI YA ACACIA YAKUBALI KULIPA DENI LAKE KWA SERIKALI

3

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania John Pombe Magufuli amesema Kampuni ya madini ya  Acacia imekubali kufanya mazungumzo na Serikali ikiwa ni pamoja na kulipa fedha ambazo Serikali inaidai kwa kufanya shughuli zake hapa nchini.
Akizungumza mara baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na Mwenyekiti wa Kampuni ya Barrick Gold Corporation inayomiliki kampuni ya Acacia Mining Limited Prof. John L. Thornton leo Ikulu jijini Dar es Salaama, Rais Magufuli amesema kampuni ya Barrick imekubali  mazungumzo na Serikali ya Tanzania na kulipa  fedha wanazodaiwa.
 “Serikali inakaribisha mazungumzo hayo na itaunda jopo la wataalamu watakaofanya majadiliano na kampuni ya Barrick Gold Corporation ili kufikia makubaliano ya kulipwa fedha zinazodaiwa na namna kampuni hiyo itakavyoendesha shughuli zake nchini kwa maslahi ya pande zote mbili” alisema Rais Magufuli
Rais Magufuli alisema kuwa licha ya kampuni hiyo kukubali  kulipa fedha wanazodaiwa Prof. John L. Thornton amekubali kushirikiana na Tanzania kujenga mtambo wa kuchenjulia dhahabu  hapa nchini.
Nae, Prof. John L. Thornton amesema kampuni yake ipo tayari kufanya mazungumzo na Serikali ya Tanzania yatakayozingatia maslahi ya pande zote mbili ikiwa ni pamoja na kulipa fedha zote ambazo inatakiwa kulipa kwa Serikali ya Tanzania.
Mazungumzo hayo kati ya Rais Magufuli na Mwenyekiti wa Kampuni ya Acacia yalihudhuriwa na Balozi wa Canada nchini  Ian Myles na Waziri wa Katiba na Sheria Prof. Palamagamba Kabudi.

No comments

Powered by Blogger.