TAMKO LA WAZIRI WA AFYA MH. UMMY MWALIMU (MB) KUHUSU UGONJWA WA KICHAA CHA MBWA KATIKA MAADHIMISHO YA KICHAA CHA MBUWA DUNIANI SEPTEMBA 28, 2017
Ugonjwa wa Kichaa cha Mbwa ni
mojawapo ya magonjwa yaliyoathiri nchi yetu na maeneo mengi duniani.
Ugonjwa huu husababishwa na virusi kutoka kwa wanyama jamii ya mbwa
ambao wameathirika na virusi hivi (Mbwa, paka, mbweha, fisi na wengineo)
na humwingia mwanadamu kwa kuumuuma na mate ya mnyama yenye virusi hivi
huingia katika eneo lenye jeraha.
Takwimu za kidunia zinaonyesha
ugonjwa wa Kichaa cha Mbwa inakadiriwa kusababisha takribani vifo 59,000
ambapo kati ya hao, asilimia 36 hutokea katika bara la Afrika.
Inakadiriwa kuwa kati ya 30%-50% ya waathirika wa kichaa cha mbwa ni
watoto chini ya miaka kumi na tano. Pamoja na kusabisha vifo, ugonjwa
huu pia unasababisha athari kubwa katika kiuchumi kwani chanjo ambayo
ndio matibabu yake ni kubwa. Gharama ya chanjo inakadiriwa kuwa 150,000
kwa mgonjwa kwa bara la AfriKa, ambayo ni sawa na 6% ya mapato ya nchi
katika bara hilo.
Kwa hapa Tanzania, ugonjwa wa
kichaa cha mbwa uliripotiwa kwa maara ya kwanza mnamo 1932/33. Baada ya
hapo, wagonjwa wameendelea kuripotiwa kutoka maeneo mbalimbali ya nchi
kwa viwango tofauti. Kwa mwaka huu kati ya mwezi Januari hadi Agosti,
watu 17,326 wametolewa taarifa ya kuumwa na mbwa au wanyama wa jamii
hiyo na kumetokea vifo 8. Takwimu hizi hazijumuishi vifo vinavyotokea
nyumbani na waathirika ambao hawakufika katika vituo vya kutolea huduma
za afya, hivyo tatizo hili ni linaweza pia kubwa kuliko tunavyofikiri.
Utafiti uliofanyika mwaka 2002 ulibainisha kuwepo na uwezekano wa kuwepo
takriban vifo 1,499 kwa mwaka nchini kutokana na ugonjwa huu.
Tafiti pia zimeonesha waathirika
wakuu wa ugonjwa huu ni watoto chini ya miaka 15. Uwezekano mkubwa ni
kwa sababu wao ndio wanaokuwa karibu na mbwa(anaefugwa) muda mwingi, na
pia hupenda kucheza/kuchokoza mbwa wasiowafahamu njiani.
Vimelea vya kichaa cha mbwa
vinapoingia katika jeraha hushambulia neva za fahamu kutoka katika eneo
la jeraha, kuelekea katika uti wa mgongo na hatimae kuathiri ubongo.
Dalili huanza kuonekana baada ya kuathirika kwa mfumo wa kati wa fahamu,
na baadae ubongo, ambazo ni pamoja na kuwashwa sehemu ya jeraha, homa,
kuumwa kichwa, maumivu ya mwili, kuogopa maji na mwanga, kutokwa mate
mengi mfululizo, kuweweseka (kushtuka mara kwa mara na kuogopa), kupooza
na hatimae kupoteza maisha. Wakati mwingine watu huhusisha dalili hizi
na imani potofu.
Katika juhudi za kudhibiti
ugonjwa huu, Tanzania ilipata ufadhili wa Bill na Melinda Gates na
kushirikiana na Shirika la Afya Duniani na kuwa moja ya nchi
zilizochaguliwa kutekeleza ‘Mradi wa majaribio wa Kutokomeza Kichaa cha
Mbwa’ kati ya mwaka 2009-2016, nchi nyingine zikiwa ni Ufilipino na
Afrika ya Kusini. Lengo kubwa la mradi huu lilikuwa ni kusaidiana na
nchi hizi katika kutokomeza ugonjwa huu kwa jamii ya mbwa na paka ili
wawe na virusi hivi endapo watamuuma binadamu. Utekelezaji wa mradi
ulihusisha kampeni za kuchanja mbwa wote kwa mwaka mara moja. Aidha,
chanjo za binadamu pia zilitolewa. Mradi huu ulitekelezwa katika mikoa
ya Dar es Salaam, Pwani, Morogoro Lindi na Mtwara, ambapo mbwa na paka
walipatiwa chanjo kila mwaka. Katika mradi huu:
- Chanjo za binadamu dozi 28,000 zilitolewa katika eneo la mradi.
- Watumishi 101 walipata mafunzo kuhusu rabies na njia mpya ya utoaji chanjo, na jinsi ya kuhakikisha hakuna ‘kuishiwa na chanjo’.
- Mwongozo wa Kudhibiti Kichaa cha Mbwa kwa wanafunzi wa shule za msingi uliandaliwa.
- Elimu ya afya kuhusu kichaa cha mbwa na jinsi ya kujikinga ilitolewa kwa jamii kupitia kampeni za uchanjaji.
- Vielimishi jamii vilitengenezwa na kusambazwa. Kufuatia mradi huu, vifo vinavyotokana na Kichaa cha mbwa katika maeneo ya mradi vilipungua toka 17 mwaka 2010 hadi 0 mwaka 2013 hadi 2015.
Kama ilivyoelezwa hapo juu,
ugonjwa huu hutoka kwa wanyama jamii ya mbwa/paka aliyeathirika na
virusi hivi na kuja kwa binadamu anapomuuma. Hivyo juhudi za pamoja
zinahitajika kwa sekta zote mbili ili kutokomeza ugonjwa huu.
Mambo muhimu ya kufanya ili kujikinga:
- Endapo mtu ameumwa na mbwa, hatua ya kwanza muhimu ni kuosha jeraha kwa dakika 10 au zaidi kwa maji mengi yanayotiririkika na sabuni. Kidonda kisifungwe. Kisha apelekwe haraka katika ktuo cha kutolea huduma za afya ili kupata chanjo ya kichaa cha mbwa. Ni muhimu aliyeumwa na mbwa afanyiwe tathmini ya kina katika kituo cha kutolea huduma ili aweze kupatiwa chanjo kamili na iwapo chanjo ikitolewa ni budi kumaliza kozi zote za chanjo. Wizara imekwisha kutoa maagizo kwa mikoa na wilaya kuhakikisha kuwa chanjo hizi zinanunuliwa na kutolewa kwa wananchi wanaozihitaji.
- Mtu aliyeumwa na kichaa cha mbwa awahi kituo cha kutolea huduma za afya na kupata chanjo dhidi ya ugonjwa huo, na ni muhimu kumaliza kozi.
- Wanyama jamii ya mbwa, paka wasiruhusiwe kulamba vidonda, kwani mate yao huweza kuleta maambukizi endapo wameathirika.
- Wamiliki wa mbwa wahakikishe wanachanja mbwa wao dhidi ya kichaa cha mbwa mara moja kila mwaka na kupata cheti.
- Mbwa wafungiwe ndani wakati wa mchana na wasiachwe kuzurura hovyo, kwani wanaweza kupata maambukizi endapo watakutana na mnyama aliyeambukizwa.
- Kuhakikisha mazingira yote ni safi, ili kutowapa chakula mbwa wanaozurura mtaani na kuzoea kuja katika mazingira tunamoishi.
- Watoto wapewe elimu na wakatazwe kuchokoza mbwa wasiowajua njiani (kuvuta mkia/masikio, kumpanda mgongoni n.k)
Katika kutekeleza mikakati na
juhudi za pamoja za sekta zote zinazohusika kudhibiti ugonjwa huu,
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto imeshirikiana na
Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Shirika la Afya Duniani, Shirika
linaloshughulika na Afya ya Wanyama Duniani (OIE) na asasi zisizo za
kiserikali katika kuandaa ‘Mkakati wa Kudhibiti Kichaa cha Mbwa’ wenye
lengo la kutokomeza ugonjwa huu ifikapo 2030.
Tunawapongeza wote wanaoshiriki
kwa njia moja au nyingine katika kudhibiti kichaa cha mbwa, na tunazidi
kutoa wito kwa jamii kwa ujumla kuzingatia maelekezo ya kuzuia/kujikinga
na ugonjwa huu. Tunatoa shukrani kwa wadau mbalimbali wanaoshiriki nasi
katika juhudi hizi- Mfuko wa Bill na Melinda Gates, Shirika la Afya
Duniani, Shirika la Wanyama, Taasisi ya Afya Ifakara na wengineo.
No comments