-MECK SADIKI:UTEUZI WA JPM KWA MGHWIRA NI SAHIHI.
ALIYEKUWA Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Said Meck Sadiki Sadiki alisema kuwa Rais hajakosea kumteua Mghwira kuwa
kiongozi wa mkoa wa Kilimanjaro kwani mwana mama huyo ni mchapakazi, mzalendo
na asiye na ubaguzi, na uongozi unahitaji mtu wa aina hiyo. “Nilimfuatilia
Mghwira katika kampeni zake akiomba urais, ni mwanamke mtulivu, mwenye mtazamo
wa maendeleo na mkoa huu wa Kilimanjaro unataka mtu atayetazama watu kwa
maendeleo na si kwa vyama,” alisema Sadiki.
Alisema kuna maeneo matano ambayo angependa mteuliwa huyo ayape
kipaumbele ikiwa ni pamoja na uharibifu wa mazingira na utunzaji wa vyanzo vya
maji. Alisema kama mazingira yataharibiwa zaidi ndani ya miaka 10 mkoa utakuwa
jangwa na na kukumbwa na baa la njaa. Katika eneo hilo, alitaka Mghwira
ashirikiane na taasisi na viongozi wengine kutunza mazingira na vyanzo vya
maji.
Eneo jingine ni uvushwaji wa bidhaa za magendo kutoka Tanzania
kwenda Kenya. Alisema mkoa unakosa mapato mengi kutokana na mbinu za ujanja za
wafanyabiashara wasio waaminifu. Alimtaka kama Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi
na Usalama ya Mkoa kujipanga vyema kudhibiti hilo. Dawa za kulevya Alisema kuwa
zimekuwa zikiathiri maendeleo ya mkoa.
Akatolea mfano Same ambako mirungi inalimwa sana na kumtaka
alishughulikie huku akiwataka wananchi kumpa ushirikiano kuwafichua wanaofanya
biashara hiyo haramu. Mimba mashuleni Alieleza kuwa mwishoni mwa mwaka jana
hadi Februari mwaka huu wamepatikana wanafunzi 38 wenye mimba kwenye wilaya ya
Same pekee. Amesema kwa kuwa mama Mghwira ni mwanamke, anayo nafasi ya
kuzungumza kwa ndani na mabinti na wanawake wasikatishe masomo.
Siasa Alisema kuwa mtu akiwa nje ya mkoa wa Kilimanjaro anaweza
akawa na mtazamo hasi wa siasa za Kilimanjaro, ila hilo si tishio kwani
anaamini kuwa kiongozi kwenye mkoa huo anashirikiana na wananchi na maendeleo
yanapatika. ACT inasemaje Wakati Sadiki akiwa alishaachia ngazi hiyo na Rais
tayari ameshamtangazia uteuzi wa nafasi hiyo mama Mghwira, Chama cha ACT
Wazalendo kimesema hatua ya Rais Magufuli kuwateua viongozi wa chama hicho
kushika nyadhifa mbalimbali katika utawala wake ni kuonesha kuwa chama hicho
kina watu wenye uwezo wa kufanya kazi nzuri na upinzani wana uwezo vile vile.
Hata hivyo, alisema uteuzi wa Rais kwa Mwenyekiti wa chama hicho
Mghwira kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, ni pigo kwa chama hicho kwani bado
kilikuwa kinamhitaji. Akizungumza na gazeti hili jana, Katibu wa Itikadi,
Mawasiliano na Uenezi wa chama hicho, Ado Shaibu alisema, “Kwetu tumepoteza
hatuwezi kusema tunafurahia uteuzi huu kwa sababu huwezi kumpa mtu keki yako
unayoipenda na wewe ukabaki na keki,” alisema Ado.
Alisema kuteuliwa kwa mwenyekiti wao kuwa mkuu wa mkoa ni
changamoto kwa chama kwani ni kiongozi wa ngazi ya juu ambaye anategemewa
kuendelea kukijenga chama. “Jambo hili lina sura mbili, kama Mghwira
tunamuachia mwenyewe atakuja kuliongelea ni jambo binafsi, “ alisema Ado. Hata
hivyo alisema Kiongozi wa chama hicho, Kabwe Zitto aliwahi kusema bungeni kuwa
katika nchi zinazoendelea kufanya kazi serikalini ni jambo ambalo linatakiwa
kufanywa na Watanzania wote bila kujali itikadi za vyama vyao ili mradi uwe na
uwezo.
“Pengine Rais ameanza kufahamu kuwa hata upinzani wana uwezo wa
kulitumikia taifa hili katika ngazi za uongozi, hata hivyo mwenyekiti wetu sasa
anachukua majukumu mapya sasa hatuwezi kumtumia kama awali katika chama chetu,
“ alisema. Ado alisema hata hivyo chama kinamsubiri mwenyekiti wao huyo ambaye
anatakiwa kufanya maamuzi aidha kupokea uteuzi huo au la.
Alisema chama cha siasa chochote kina malengo yake ni kushika
dola na kuongoza kwa ilani na namna ambavyo wanaona inafaa tofauti na sasa
Mghwira ataongoza kwa matakwa ya Chama Cha Mapinduzi kilichomteua. “Hata kama
mama atakuwa kiongozi sasa hawezi kutekeleza ilani ya ACT, kwa hiyo hatuwezi
kusema kama uteuzi huu ndani ya chama umetufurahisha,” alisema Ado.
Alipotafutwa Mghwira hakupatikana ambapo ilielezwa kuwa yuko nje
ya nchi na anatarajiwa kurudi leo na kiongozi wa chama hicho, Zitto alisema
hajawa na muda wa kuzungumza katika jambo hilo. Hata hivyo, jana jioni kupitia
kwenye ukurasa wake wa mitandao ya kijamii (Facebook), Zitto aliandika,
“Nimekuwa naulizwa sana kuhusu uteuzi wa mwenyekiti wa chama chetu kuwa Mkuu wa
Mkoa wa Kilimanjaro.
Nimekuwa kimya kwa sababu tumepokea taarifa za uteuzi huo kutoka
katika vyombo vya habari. Mwenyekiti yuko nje ya nchi na kutokana na tofauti za
saa hatujawasiliana naye. Tutatoa tamko kamili atakapokuwa amerejea nchini...
“...Ninawataka wanachama wote wa ACT Wazalendo wawe watulivu na kama kuna
masuala yanayohusu maamuzi ya vikao vya chama tutawajulisha.
“
Aliyeteuliwa ni Mwenyekiti wa chama Taifa, sio mshauri au mwanachama tu. Ni
mmoja wa viongozi wa juu wa Chama chetu. Uteuzi wake unahitaji kikao cha kamati
kuu ya chama kukaa na kujadili. Nitaweza kutoa taarifa baada ya vikao vya
kamati Kuu. Kwa sasa umma usubiri vikao Kwa mujibu wa Katiba ya Chama chetu.”
Juzi Rais Magufuli alimteua Mghwira kuwa mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro kushika
nafasi ikiyoachwa wazi na Said Meck Sadick ambaye alijiuzulu wadhifa huo. Mbali
na Mghwira, kiongozi mwingine wa chama hicho aliyeteuliwa na Rais ni Profesa
Kitila Mkumbo aliyeteuliwa Aprili 4 mwaka huu, kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya
Maji na Umwagiliaji.
No comments