MICHUANO YA MAZINGIRA KABUMBUMBU CUP 2017 KUZINDULIWA KESHO WILAYANI BAGAMOYO
Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Majid Mwanga akiwa na baadhi ya askari Mgambo wakiwa wanashiriki katika moja ya zoezi la kufanya usafi.
……………….......................
MKUU wa Wilaya ya Bagamoyo Majid Mwanga katika kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Dk. John Magufuli katika kukuza michezo hapa nchini ameamua kuandaa mashindano maalumu ya mchezo wa soka ambayo yatazishiriikisha jumla ya timu 28 kutoka kata 26 zilizopo Wilayani humo yaliyopewa kwa jina la ‘Mazingira kabumbu Cup 2017’.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Majid alisema kwamba Michuano hiyo inatarajiwa kuanza kutimua vumbi lake Julai 15 katika uwanja wa Mwanakalenge ambapo lengo kubwa na kuanzisha mashiindano hayo ni kwa ajili ya kuweza kuwakutanisha vijana na viongozi mbali mbali wa serikali pamoja na wabunge,na madiwani katika kuwahimiza suala zima la utunzaji wa mazingira sambamba na kushiriki kikamilifu katika kufanya usafi.
Pia alifafanua kuwa katika mashindano hayo pia yatawajumisha viongozi wengine wa serikali kutoka idara mbali mbali pamoja na kuwashirikisha madiwani na wabunge wote kutoka halmashauri zote mbili za Bagamoyo pamoja na Chalinze ili kuweza kushiriki katika mashindano hayo ambayo yatakwenda sambamba na kuweka mikakati kabambe ya kuweza kutunza vyanzo vya maji,kutunza afya,pamoja na mazingira.
“Kitu kikubwa ninachopenda kukisema ofisi ya Mkuu wa Wilaya tumeona ni vema kumuunga mkono Rais wetu wa awamu ya tano John Magufuli katika kutunza na kufanya usafi wa mazingira sambamba na agizo la Makamu wa Rais la Mama Samia Suluhu Hassan la kufanya mazoezi ya michezo kila mwisho wa mwezi tumeamua kuandaa michuano hiyo ambayo itajulikana kama Mazingira kabumbu Cup 2017,”ambayo itaenda sambamba na zoezi la kufanya usafi wa mazingira.
Majid alibainisha kuwa mshindi wa kwanza katika mashindano hayo atajinyakulia zawadi ya Piki piki ya matairi matatu aina ya Toyo ambayo pia itaweza kutumika katika shughuli mbali mbali za kuweza kusaidia kwa kiasi kikubwa kusombea taka taka kwa lengo la kuweza kuyaweka mazingira katika hali ya usafi .
Aidha alisema kwamba ana imani kwamba kufanyika kwa mashindano hayo Wilayani Bagamoyo kutaweza kuwapa fursa wachezaji wengine ambao walikuwa hawapati fursa ya kuweza kuonyesha vipaji vyao walivyonavyo katika kulisakata kabumbu.
Katika hatua nyingine Majid alisema kwamba katika mchezo wa ufunguzi wa mashindano hayo utazikutanisha timu ya madiwani ambao wataungana na wabunge wote waili kutoka halmashauri zote mbili za Chalinze na bagamoyo ambao watamenyana vilivyo na timu ya wakuu wa idara kutoka ofisi ya Mkuu wa Wilaya.
Pia Majid aliwaomba wadau wa mchezo wa kabumbu pamoja na wananchi wa Wilayanai Bagamoyo kujitokeza kwa wingi siku hiyo kwa ajili ya kushiriki kikamilifu katika zviwanja hivyo vya Mwanakalenge pamoja na kujitokeza katika kufanya usafi wa mazingira katika maeneo mbali mbali ili kuweza kutekeleza agizo la Rais Dk.John Magufuli
No comments